Mkutano wa kwanza wa Jukwaa la Wanawake katika usafiri wa anga Tanzania (T-WIA) ukiwakutanisha wanawake viongozi katika sekta ya Usafiri wa Anga nchini umefanyika nchini.
Mhe. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Riziki Juma Pembe amefungua mkutano huo Oktoba 31,2024 jijini Dar es Salaam na kutoa pongezi kwa wanawake kwa juhudi wanazozifanya katika kujipambanua katika usafiri wa anga.
Katika hotuba yake, Mhe. Riziki alisisitiza juu ya umuhimu wa serikali kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa katika sekta zote. Aliongeza kuwa, kila mtu anapaswa kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo yake, huku akitoa wito kwa wanawake kuwa na ujasiri na kujituma katika kufanikisha ndoto zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw. Salim Msangi, alisema anatambua mchango muhimu wa wanawake viongozi katika jukwaa hilo na kuahidi kuendelea kuwapatia ushirikiano wa karibu ili kufanikisha malengo waliyojiwekea.
Naye Bi. Maria Memba, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TCAA na mwanzilishi wa Jukwaa hilo alibainisha kuwa kifanyika kwa mkutano huo ni mwanzo tu wa safari ndefu ya kuwawezesha wanawake katika sekta ya usafiri wa anga.
Bi Memba, alisisitiza juu ya umuhimu wa kuendelea kuhamasisha wanawake kushiriki kikamilifu katika ngazi ya uongozi na maamuzi kwenye sekta hiyo. Aliongeza kuwa, jukwaa hilo linalenga kuleta mabadiliko chanya na kuhakikisha kunakuwa na uwakilishi sawia baina ya jinsia katika usafiri wa anga Tanzania.
Jukwaa hilo lilizinduliwa rasmi mnamo mwaka 2023 jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 20 ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini.