Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imekabidhi cheti cha kuipasisha Kampuni ya Airplane Africa Limited (AAL) ambayo ni ya kwanza hapa nchini inayounda na kutengeneza ndege iliyopo Mazimbu mkoani Morogoro.
Akikabidhi cheti hicho kwa uongozi wa Kampuni hiyo inayomilikiwa na wawekezaji kutoka Jamhuri ya Czech, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Salim Msangi amesema haya ni matokeo ya kaguzi zilizokuwa zikifanywa na wakaguzi wa TCAA ili kuhakikisha shughuli zinazofanyika katika kiwanda hicho zinafuata utaratibu ili kuwezesha uzalishaji wenye ubora utakaopokelewa vyema katika soko.
Bw. Msangi ameupongeza uongozi wa AAL kwa kufuata taratibu zote muhimu na kuoneshwa kufurahishwa na namna ambavyo wahandisi wazawa wamepewa kipaumbele na kujengewa uwezo katika uundaji wa ndege hizo.
"Nipende kuwashukuru kwa kuichagua Tanzania kama sehemu ya kuwekeza kwakuwa mngeweza kwenda popote Afrika lakini mkaamua kupachagua hapa na sasa historia inawekwa kwa AAL kuwa kampuni ya kwanza kuuunda na kutengeneza ndege hapa nchini. Vile vile niwapongeze kwa mambo mawili, moja ni ushirikiano na utayari wenu katika kufuata utaratibu wote wa vibali na kaguzi za kitaalam na pili ni namna ambavyo mmewapa nafasi wahandisi wetu wazawa kuwa sehemu ya historia hii njema katika sekta ya usafiri wa anga hapa nchini. TCAA itaendelea kushirikiana nanyi ili kuendeleza mipango yenu mizuri ya uwekezaji katika sekta hii" alisema Bw. Msangi.
Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Igor Stratl ameishukuru TCAA kwa ushirikiano waliowaonesha hadi kufikia hatua hii muhimu ya kuwapasisha na kuwakabidhi cheti hicho na kuongeza kuwa wamevutiwa kuwekeza Tanzania kwa sababu ni nchi yenye usalama, utulivu, amani na hivyo imewarahisishia kufanya kazi zao muda wote.
Kiwanda hicho kilichoanza mwaka 2021 mpaka sasa kimeunganisha na kutengeneza ndege zaidi ya tatu zenye uwezo wa kubeba abiria wawili na sasa zinaweza kuuzwa katika nchi mbalimbali ambapo mipango ijayo ni kuunda ndege zenye kuchukua abiria kuliko idadi ya wawili wa sasa.