TAARIFA KWA UMMA

 

 

 

 

 

MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA TANZANIA

 

              DAR ES SALAAM                                                                                       21 Novemba 2018

 

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAFUNZO YA URUBANI KATIKA CHUO CHA TANZANIA AVIATION UNIVERSITY COLLEGE (TAUC)

 

 

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) inapenda kuufahamisha umma wa watanzania kuwa Chuo cha Tanzania Aviation University College (TAUC) kilichopo Tabata, Dar es salaam kimepewa hati ya uthibitisho wa kutoa mafunzo ya Maafisa wa Huduma katika kampuni za ndege Flight Operations Officers (FOO)/Flight Dispatcher pekee. Hivi karibuni, Mamlaka imepata taarifa za kuaminika kuwa Chuo cha Tanzania Aviation University College (TAUC) kinatangaza kuwa kinatoa mafunzo ya urubani kinyume na vigezo na masharti ya cheti ilichopewa na Mamlaka kutoa mafunzo kwa mujibu wa kanuni za Civil Aviation (Approved Training Organization) regulations, 2017.

 

Kutokana na yaliyojiri, Mamlaka iliwasiliana na uongozi wa Tanzania Aviation University College (TAUC) ikiwamo kuchukua hatua kwa mujibu wa kanuni na taratibu kama  inavyoainishwa katika kanuni ya 46 ya Civil Aviation (Approved Training Organization) Regulations, 2017. Kwa muktadha huu, Mamlaka ilitoa onyo kali kwa uongozi wa Tanzania Aviation University College (TAUC) ili kuacha mara moja kuendelea kuvunja kanuni na kukiuka vigezo na masharti ya cheti walichopewa na Mamlaka katika kutoa mafunzo katika sekta ya anga.

 

Kwa taarifa hii, tunautaarifu umma kuwa Chuo cha Tanzania Aviation University College (TAUC) hakijathibitishwa na hakijaidhinishwa kutoa mafunzo ya urubani kama inavyotangazwa na Chuo hicho kupitia vyombo mbalimbali vya habari. Kwa mujibu wa kanuni ya 45 ya Civil Aviation (Approved Training Organization) regulations, 2017, Mamlaka inapenda kuushauri umma wa watanzania kutoa taarifa kuhusu uvunjwaji wowote wa kanuni katika utoaji wa mafunzo katika sekta ya anga mahali popote.

 

 

Mamlaka iko katika taratibu za kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Chuo cha Tanzania Aviation University College (TAUC) kwa madhumuni ya kulinda maslahi ya umma, kuimarisha usalama wa anga na kusimamia weledi na umahiri wa wataalamu katika sekta ya anga nchini mwetu.

 

 

Imetolewa na

MKURUGENZI MKUU

MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA TANZANIA